Tarehe 14 Juni 2026, Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, alifanya mazungumzo na Dkt. Mohamed Khelifa, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Viwanda vya Bidhaa za Umeme nchini Algeria (CIEL) na Meneja Mkuu wa kampuni ya umeme ya GISB katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers.

 

Kikao hicho ni matokeo ya ziara ya Dk. Khelifa nchini Tanzania ambako mbali ya kushiriki Mkutano wa Uwekezaji Zanzibar 2026, alikutana pia na mamlaka mbalimbali za nishati na madini nchini.

 

Kwa upande wake, Dkt. Khelifa alimweleza Mhe. Balozi kuhusu matokeo chanya ya zira hiyo na jinsi alivyovutiwa na mazingira ya uwekezaji pamoja na fursa zilizopo Tanzania.

 

“Nimefurahi sana kutembelea Tanzania na  napenda kuuchukua fursa hii kuushukuru Ubalozi kwa uratibu mzuri wa miadi na taasisi za REA, TANESCO, ZECO na TPDC pamoja na Wizara ya Madini. Tumepata nafasi ya kujadili mambo mengi ya ushirikiano kwenye sekta ya nishati na madini ikiwemo eneo la uwekezaji na kubadilishana uzoefu”, alisema Dkt. Khelifa.

 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Khelifa amemtaarifu Mhe. Balozi kuwa anaratibu ujumbe wa kampuni za Algeria za umeme kutembelea Tanzania mwezi Julai na kushiriki maonesho ya Sabasaba.

 

Kwa upande wake Mhe. Balozi alimshukuru Dkt. Khelifa kwa ziara yake nchini Tanzania na dhamira yake ya dhati ya kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la nishati na madini. Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alimhakikishia Dkt. Khelifa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.