Tarehe 05 Mei 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alikutana kwa lengo la kumuaga Mhe.  Ahmed Attaf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Algiers.

Mhe. Balozi Njalikai alitumia Mkutano huo kuishukuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria hususan Rais wa Jamhuri Mhe. Abdelmadjid Tebboune kwa kuridhia maombi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumwakilisha katika nchi hiyo.  

Mhe. Balozi pia alimshukuru Mhe. Waziri na Wizara ya Mambo ya Nje kwa ushirikiano thabiti  waliompatia katika muda wote alokuwa akitekeleza  majukumu yake ya Kidiplomasia na kujenga uhusiano imara kati ya Tanzania na Algeria.

Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi amemuomba Mhe. Waziri kuendelea kumpa ushirikiano Balozi Mpya katika kuhakikisha kuwa uhusiano wa Algeria na Tanzania unaimarika zaidi kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mhe. Waziri amempongeza Mhe. Balozi kwa kazi kubwa aliyoifanya hususan katika kuimarisha uhusiano wa uwili na diplomasia ya uchumi na kuahidi kuwa kwa msingi ulojengwa wa ushirikiano anayo imani kubwa kuwa mrithi wake atapata nafasi nzuri ya kuendeleza ushirikiano huo.

Sambamba na hilo, Wizara ya Mambo ya  nje ilimshukuru na kumtakia heri na mafanikio katika majukumu yake mapya atakayopangiwa.