Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, katika ziara yake jijini Oran, alipata fursa ya kukutana na wanafunzi Tanzania wanaosoma katika katika miji ya Oran, Mostagenem na Mascara ikiwa ni sehemu ya kufahamu maendeleo ya masomo yao na changamoto zinazowakibili ili kuzitafutia ufumbuzi.

 

Mhe. Balozi Matinyi alianza kukutana na wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi stadi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) mjini Mascara wakati akielekea Oran mnamo tarehe 4 Oktoba, 2026,

 

Akiwa jijini Oran, Mhe. Balozi Matinyi alikutana na wanafunzi wa jijini hapo Oran na Mostagenem wanaosomea masomo udaktari, Tehama  na ukalimani wa lugha za Kiarabu, Kifaransa na Kingereza. 

 

Baada ya kusikiliza maendeleo na changamoto zao za kimasomo, Mhe. Balozi Matinyi, aliwataka wasome kwa bidii ili baada ya kuhitimu warejee kurudi nyumbani kulihudumia taifa. 

 

Aidha, aliwataka wawe karibu na Ubalozi na kuelezea kila changamoto inayokabili zikiwemo za vibali na ukaazi na kutoa taarifa mapema ili Ubalozi uwapatie msaada kwa wakati.

 

Vilevile, Mhe. Balozi Matinyi aliwafahamisha wanafunzi hao kuwa kwa mwaka huu wa masomo 2026/2027, Ubalozi unatarajia kupokea wanafunzi 150 kutoka Tanzania; na hivyo kuwataka waoneshe uzalendo na kuwapa ushirikiano mara watakapowasili nchini Algeria.