Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akiwa ziarani mkoani Oran alipata nafasi ya kuitembelea kampuni ya uzalisahaji wa mazulia, nyasi chotara na nyasi bandia ya Tapis D’or mnamo tarehe 6 Oktoba, 2026.
Kampuni hiyo ya Tapis D’or ilianzishwa mwaka 1983 na yenye wafanyakazi 1,600, huzalisha mita za meaba milioni 30 za mazulia kwa mwaka na zaidi ya mita za mraba milioni saba za nyasi bandia na vilevile tani 16,000 za nyuzi kwa mwaka.
Wateja wakubwa wa Tapis D’or ni wananchi wa kawaida nchini Algeria, kampuni binafsi, hoteli, nyumba za ibada na viwanja vya mipira. Kwa upande wa soko la nje tayari Tapis D’or inauza bidhaa zake katika nchi za Ujerumani, Ubelgiji, Uswizi, Poland, Kanada, Ufaransa, Chile, Equador, Korea Kusini, Saudi Arabia, Libya, Core d’Ivoire, Nigeria na Senegal.
Akizungumza na Mhe. Balozi Matinyi, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Tapis D’or, Yahya Ballalou, na Mkurugenzi wa Mauzo ya Nje, Hammou Boussada, alieleza mafanikio ya kampuni hiyo kuwa ni kampuni pekee barani Afrika yenye ithibati ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (FIFA) katika utengenezaji wa nyasi bandia.
Aidha, Tapis D’or pia imewahi kusimamia upandaji wa nyasi chotara katia viwanja vitatu vyenye hadhi ya FIFA nchini Algeria ukiwemo uwanja wa kisasa wa Nelson Mandela, jijini Algiers.
Katika kutanua wigo wa biashara, Tapis D’or imeweka wazi utayari wa kuitembelea Tanzania kwa ili kuangalia fursa zaidi za biashara ya mazulia na viwanja vya michezo na kukuza ushirikiano na vyama vya wafanyabiashara wa Tanzania.



