Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi akiwa pamoja na ujumbe wa Kampuni ya Uuzaji na Usambazaji wa Bidhaa za Mafuta Tanzania (TANOIL), walishiriki katika Maonesho ya 14 ya Nishati na Haidrojeni Afrika na Mediterania (NAPEC), yaliyofanyika tarehe 5-7 Oktoba, 2026, jijini Oran nchini Algeria.

 

TANOIL iliyowakilishwa na Kaimu Meneja Mkuu, James Sanawa, na Mkuu wa Masoko na Uwekezaji, Neema Mwasha, ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na ilituma ujumbe wake huo nchini Algeria ili kutafuta fursa za ushirikiano. 

 

Maonesho hayo yaliyojumuisha kongamano lililohutubiwa na viongozi wa Serikali ya Algeria na kampuni kubwa za kimataifa, yalihudhuriwa kampuni mbalimbali za nishati duniani ikiwemo za Eni, Oxy, PTTEP, Midad Energy, Sonatrach, Total Energy, 

 

Mhe. Balozi Matinyi na ujumbe wa TANOIL walifanya mazungumzo na Shirika la Mafuta na Gesi la Algeria (SONATRACH)) ambalo liliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Yasmine Boukacem, na Meneja wa Masoko wa Gesi, Naima Benhamida, kuhusu mawanda mapya ya ushirikiano, hususan katika biashara ya gesi (LPG) kwa ajili ya matumizi ya nishati safi nchini Tanzania. 

 

Kadhalika, ujumbe wa Tanzania ulifanya mazungumzo na NAFTAL, ambayo ni kampuni tanzu ya SONATRACH inayoshughulika na usambazaji wa mafuta na bidhaa zake. Pande zote mbili zilijadili kuhusu biashara ya vilainishi vya mitambo na utengenezaji wa mitungi ya gesi kwa ajili ya soko la Tanzania pamoja na kuikaribisha NAFTAL kufanya ziara Tanzania.

 

Aidha, TANOIL ilipata nafasi ya kufanya mazungumzo na kampuni mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi kama vile kampuni ya ZEECO ya Marekani na SEGITEC ya Tunisia kuhusiana na ushirikiano katika uwekezaji na bishara nchini Tanzania na katika soko la nchi za mashariki, kati na kusini mwa Afrika.