Kampuni mbalimbali za Algeria zinazojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kilimo zimeonesha nia ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na Tanzania kwa kutafuta wabia katika sekta mbalimbali za uzalishaji, biashara na viwanda.
Nia hiyo imejitokeza wakati wa Maonesho ya 57 ya Biashara ya Kimataifa ya Algiers (FIA), yaliyofunguliwa rasmi tarehe 22 Juni 2026 na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, katika Kituo cha Maonesho cha Shirika la Maonesho na Biashara ya Nje la Algeria (SAFEX).
Akizungumza katika banda la Tanzania siku ya pili ya maonesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, alisema kuwa kampuni kadhaa za Algeria zimeonesha dhamira ya kuanzisha ushirikiano wa moja kwa moja na Tanzania. Miongoni mwa kampuni hizo ni GISB, inayotarajia kuuza vifaa vya umeme nchini na kuwekeza katika uzalishaji wa nyaya za umeme kwa kutumia shaba inayozalishwa Tanzania, pamoja na GETEX inayotafuta fursa za kununua katani na pamba huku ikipanga kuwekeza katika sekta ya usindikaji wa bidhaa za ngozi.
“Afisa Mtendaji Mkuu wa GISB, Dkt. Mohamed Khelifa, anatarajiwa kufanya ziara nyingine nchini mwezi Julai 2026 kufuatia ziara yake ya awali ya mwezi Mei mwaka huu. Aidha, viongozi wakuu wa kampuni tatu tanzu za GETEX wanakusudia kutembelea Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL) mwezi Oktoba 2026 ili kujionea fursa za ushirikiano wa uwekezaji,” alisema Balozi Matinyi.
Kampuni nyingine zilizoonesha nia ya kushirikiana na Tanzania ni pamoja na Tapidor inayozalisha mazulia na nyasi bandia za viwanja vya michezo, Optimaflex inayotengeneza magodoro, Géant Electronics inayojihusisha na bidhaa za umeme, Bellat inayofanya shughuli za usindikaji wa nyama na ujenzi wa makazi, pamoja na SARL CPC inayotafuta soko la dagaa wa baharini na samaki aina ya jodari kutoka Tanzania. Kwa mujibu wa Balozi Matinyi, Meneja Mkuu wa SARL CPC, Samir Benhamada, anatarajiwa kutembelea Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) mwezi Julai 2026 kwa mazungumzo ya ushirikiano wa kibiashara.
Balozi Matinyi alibainisha kuwa soko la Algeria lina mahitaji makubwa ya bidhaa za kilimo na mifugo kutoka Tanzania, zikiwemo kahawa, korosho, ndizi, maharage ya soya, mchele, maziwa ya unga pamoja na nyama za ng’ombe, mbuzi na kondoo. Alitolea mfano mahitaji makubwa ya nyama nchini humo wakati wa Sikukuu ya Idi Al-Adha, ambapo Serikali ya Algeria hivi karibuni iliagiza kondoo milioni moja kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Maonesho hayo, makubwa zaidi nchini Algeria, yamewakutanisha jumla ya kampuni 731, zikiwemo kampuni 549 za Algeria kutoka sekta mbalimbali za uchumi na kampuni 202 za kimataifa kutoka nchi 36, ambapo nchi 16 zinatoka bara la Afrika.
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, Tanzania inaendelea kutangaza vivutio vyake vya utalii vinavyojumuisha hifadhi za wanyamapori, fukwe za Bahari ya Hindi, milima, urithi wa kihistoria na utamaduni wake wa kipekee. Aidha, nchi inawasilisha fursa za uwekezaji katika sekta za madini, viwanda, kilimo, nishati, uchukuzi na biashara.
Mbali na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria, taasisi nyingine za Serikali zinazoshiriki maonesho hayo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), inayowakilishwa na Meneja wa TEHAMA na Takwimu, Robert Mtendawema, pamoja na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), inayowakilishwa na Kaimu Mhasibu Mkuu Gilbert Lyimo na Afisa Hesabu Mkuu Omary Mafita.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania
Algiers, Juni 23, 2026



