Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi,  amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mauzo wa kampuni ya uzalishaji dawa za tiba ya Frater Razes ya Algeria, Bw. Zaki Hamdani, katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers tarehe 11 Juni, 2026.

 

Katika kikao viongozi hao wawili walizungumzia fursa za ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji nchini Tanzania kupitia Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) na kampuni tanzu ya MSD ya uzalishaji dawa ya Medipharm.

 

Kampuni ya Frater Razes imesema kwamba imeshawishika kuwekeza na kufanya biashara na Tanzania, na kwamba tayari ipo katika mazungumzo ya awali na mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).

 

Mhe. Balozi Matinyi alimweleza Mkurugenzi Hamdani kwamba kuna fursa kubwa ya soko nchini Tanzania pamoja na soko la nchi za kusini na mashariki mwa Afrika kupitia Tanzania. Balozi Matinyi alimhakikishia ushirikiano wa kutosha wa Serikali kwani imejipanga kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa kutoka asilimia 20 hadi asilimia 70 ifikapo mwaka 2030.

 

Frater Razes ni moja ya kampuni kubwa za uzalishaji dawa za tiba ya binadamu nchini Algeria ikizalisha zaidi ya aina 150 za dawa na kufanya biashara na zaidi ya mataifa 25. Hivi sasa inaendelea na utafiti wa dawa mpya zaidi 100.