Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO), Bw. Raymond Mbilinyi, ameahidi kushirikiana na Shirika la Umeme na Gesi la Algeria (SONELGAZ) katika teknolojia ya kisasa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuboresha huduma hiyo nchini.
Akizungumza na Balozi Mobhare Matinyi katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers tarehe 25 Julai, 2026, Bw. Mbilinyi alisema ziara yao ya wiki moja imewapatia mwanga kuhusu teknolojia ya kisasa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme inayozingatia ubora wa huduma na utunzaji wa nishati.
Bw. Raymond alimfahamisha Balozi Matinyi kwamba kupitia ziara hii waliona fursa nyingi za ushirikiano na Sonelgaz kupitia kampuni yake ya Sonelgaz International ambayo inaendelea na miradi ya umeme nchini Msumbiji, Chad, Niger, Senegal, Cote d’Ivoire na Tunisia.
Kwa upande wake, Balozi Matinyi alilisitiza umuhimu wa taasisi za nishati nchini kuja Algeria kujifunza, kubadilishana uzoefu na kubuni mikakati ya ushirikiano katika maeneo ambayo Algeria imepiga hatua kubwa.
Akigusia maendeleo ya sekta ya nishati nchini Algeria, Balozi Matinyi alidokeza kwamba asilimia 99 ya nchi ya Algeria imeunganishwa na umeme na asilimia 70 imeunganishwa na mtandao wa gesi wakati Sonelgaz huzalisha megawati 26,000 za umeme.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) iliyopo Arusha, Profesa David Kalaba, aliushukuru Ubalozi kwa kushirikiana nayo katika kuratibu ziara hiyo iliyojumuisha kutembelea viwanda vya vifaa vya umeme vya kampuni ya GISB jijini Mostaganem.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Julai 20, 2026.
