Tarehe 5 Novemba 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alitembelea kiwanda cha Nguo cha S.P.A Tayal kilichopo mkoani Ghelizani nchini Algeria. S.P.A Tayal ni moja ya Viwanda vikubwa vya nguo barani Afrika chenye ukubwa wa ekari 110 na wafanyakazi wapatao 4,000. 

Kupitia ziara hiyo, Mhe. Balozi alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Bw. Tarik Ekerbicer kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Kampuni ya S.P.A Tayal na wadau wa sekta ya pamba na nguo nchini Tanzania.

 Kwa upande wake Bw. Tarik alieleza utayari wao wa kushirikiana na Tanzania na kuangalia uwezekano wa upatakinaji wa mali ghafi (pamba) pamoja na kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa zao. Kwa sasa kampuni hiyo inaagiza pamba kutoka mataifa mbalimbali ya Amerika na Ulaya. 

Kampuni ya S.P.A Tayal ni wazalishaji wa vitambaa na nguo ambapo hufanya kazi na kampuni kubwa za kimataifa kama vile Zara, Celio, Levis, Decathlon, Marcopolo nk. Aidha, Kampuni inazalisha majora ya vitambaa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya viwandani ikiwemo ikiwemo uzalishaji wa nguo za vyombo vya ulinzi na usalama na zimamoto. 

Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa vitambaa na ushoni, Mhe. Balozi alipata pia fursa ya kujionea bidhaa hususan nguo zinazozalishwa na Kampuni hiyo zilizo tayari kwa ajili ya usambazaji hususan kwenye masoko ya ulaya na Asia. 

Kupitia ziara hiyo, Mhe. Balozi ameishauri Kampuni ya S.P.A Tayal kufanya ziara rasmi ya kikazi nchini Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa zilizopo kuanzia kwenye malighafi ya nguo hasa pamba, soko la bidhaa zao na uwezekano wa kufanya uwekezaji. Aidha, wawili hao walikubaliana kuratibu ziara ya ujumbe wa Tayal kwenda Tanzania mwishoni mwa Januari au mwanzoni mwa Februari 2026.