Tarehe 14 Januari 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alitembelea Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Boti "ECOREP SPA" iliyopo Mkoani Tipaza.

 Ziara hiyo ililenga kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Kampuni hiyo pamoja na uwezo wake wa ujenzi na ukarabati wa boti sanjari na teknolojia inayotumika. Aidha, baada ya kutembelea na kujionea shughuli za ujenzi na ukarabati wa meli na boti zinazoendeshwa kwenye karakana hiyo zilizopo katika Bandari Kuu ya Uvuvi ya Bouharoun Mkoani Tipaza, Mheshimiwa Balozi pamoja na mwenyeji wake Bw. Benderradji Hamid, Mwenyekiti wa ECOREP SPA walifanya mazungumzo ambayo pamoja na mambo mengine yaliangazia uwezekano wa kampuni hiyo kushirikiana na Taasisi muhimu za Tanzania katika eneo la ujenzi na ukarabati wa boti ili kuchagiza maendeleo ya sekta ya uchumi wa buluu. 

Mwenyekiti huyo wa ECOREP SPA alieleza kuwa kampuni hiyo iliyoanzishwa miaka 45 iliyopita, imeendelea kujiimarisha na kuongeza wigo wa shughuli zake za ujenzi na ukarabati wa boti za ukubwa na aina mbalimbali zikijumuisha matumizi ya aluminium, chuma, fiber na mbao. Kampuni ya ECOREP ni watengenezaji wa boti za uvuvi kuanzia urefu wa mita nne (4.8) hadi mita arobaini (40). Boti za kukokota meli (tagi) zenye urefu wa mita 13.85 zenye uwezo wa hp2x250, ASD Tagi mita 30 na 2x1360. Boti maalum za uvuvi wa jodari zenye urefu wa mita 32 na zaidi na nguvu ya uendeshaji ya 1000hp, boti za kitalii mita 16.50, uwezo wa kupakia abiria 8+64 na boti za abiria (ferry) mita 39 zenye uwezo kupakia abiria 300. 

Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi alimueleza Mwenyekiti wa Kampuni ya ECOREP kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania katika eneo la bahari ya Hindi na maziwa makuu pamoja na sera ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu na kwamba mamlaka za Tanzania zipo tayari kufanya kazi na ECOREP SPA katika eneo hilo la uchumi wa buluu. 

Mhe. Balozi ameiomba Kampuni ya ECOREP kufanya ziara rasmi nchini Tanzania kwa ajili ya kukutana na Taasisi muhimu zinazoshughulika na ujenzi na ukarabati wa boti ili kuona namna bora ya kuwa na ushirikiano wa pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili.