Tarehe 6 Novemba 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai aliungana na Mabalozi wa Nchi mbalimbali na Viongozi wa Serikali katika Ufunguzi wa Maonesho ya 10 ya Kimataifa ya Uvuvi na Ufugaji wa majini yanayojulakana kama SIPA 2025 ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili jijini Oran nchini Algeria.

 

Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 6 Novemba 2025 yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo, Maendeleo ya Vijijini na Uvuvi, Mhe. Yacine El Mahdi Oualid na Mgeni wa heshima, Waziri wa Kilimo na Uvuvi  na Rasilimali Maji wa Oman, Dr. Saud bin Hamoud Al Habsi ambaye aliambatana na ujumbe muhimu kutoka Oman.

 

Kupitia jukwaa hilo muhimu, Mhe. Balozi alifanya mazungumzo na Kampuni mbalimbali za Algeria ikiwemo kampuni ya ECOREP na kampuni ya Raphia Ficelles kungalia fursa za ushirikiano na Tanzania hususan katika eneo la utengenezaji wa boti za uvuvi ikiwemo uvuvi wa bahari kuu.

 

Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kuainisha fursa mbalimbali za uchumi wa buluu zilizopo nchini Tanzania kuanzia uvuvi wa Bahari Kuu ambapo Tanzania imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la ukanda wa bahari wenye zaidi ya kilomita 1,400. Eneo jingine ambalo Mhe. Balozi alilitilia mkazo ni pamoja na fursa za ufugaji wa samaki wa maji chumvi na maji baridi kwa kutumia teknolojia ya vizimba, uzalishaji wa chakula cha samaki na vifaranga bora.

 

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alitembelea banda la Kampuni ya Jeshi la Maji la Algeria, watengenezaji na wakarabati wa boti za uokozi, boti za kuongoza meli pamoja  na boti za kukokota meli (Tagi) kama eneo  muhimu kwa Tanzania  kubadilishana uzoefu.

 

Ushiriki wa Ubalozi katika tukio hili umekuwa na umuhimu wa kipekee ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa za uvuvi zilizopo nchini Tanzania pamoja na kubadilishana uzoefu na wenyeji ambao wamepiga hatua katika utengenezaji wa boti za uvuvi na ufugaji wa samaki wa kisasa unaoendana na mabadiliko ya tabianchi.