Leo tarehe 23 Novemba 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Bohari Kuu ya Dawa nchini Tanzania (MSD) uliombatana na wajumbe wa Kampuni Tanzu ya Medipharm pamoja wajumbe kutoka Mamlaka ya Usajili wa Dawa na Vifaa Tiba nchini Tanzania (TMDA) katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers.
Ujumbe huo, upo nchini Algeria kwa ajili ya kuangazia fursa mbalimbali za ushirikiano kati ya Taasisi za Umma na Binafsi za Algeria katika uagizaji, ufungashaji na uzalishaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba. Algeria imepiga hatua kubwa kwenye eneo hilo kwani uzalishaji wa ndani wa dawa ni zaidi ya asilimia 80.
Kwa upande wake Mhe. Balozi aliweka wazi uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Algeria na kutilia mkazo fursa zilizopo upande wa afya na dawa za binadamu. Mhe. Balozi alisisitiza kuwa Tanzania inayo nafasi kubwa ya kujifunza kutoka Algeria katika sekta ya Dawa na kuonesha utayari wa Kampuni za Algeria kusajili dawa zao na kufanya biashara na Tanzania itakayoambatana na mipango ya uwekezaji.
Kwa upande mwingine, ujumbe huo wa Serikali ulipata nafasi ya kutembelea kiwanda cha dawa cha *Biocare Group* wazalishaji wa kwanza wa dawa aina ya *insuline* nchini Algeria. Ujumbe huo, ulipata fursa ya kujifunza kuhusu taswira ya maendeleo ya viwanda vya dawa nchini Algeria.
Sambamba na hilo, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye eneo hilo kwa kuanza na maazimio ya kuunda Timu ya Pamoja itakayoandaa mapendekezo ya makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara unaolenga ununuzi na ufungashaji wa dawa na mpango wa muda mrefu wa uzalishaji wa Dawa nchini Tanzania kupitia MSD na MSD Medipharm.





