Tarehe 9 Novemba 2025 Mhe. Iman Njalikai, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, alitembelea na kufanya Mazungumzo na Kampuni ya GISB Electric iliyopo Mkoani Mostaganeme Nchini Algeria. Ziara hiyo ni sehemu ya muendelezo wa kuimarisha ushirikiano na Taasisi zinazounda Kongani ya Viwanda vya Umeme nchini Algeria (CIEL).

 

Algeria imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya umeme ikiwemo uzalishaji wa vifaa vya umeme kuanzia *gas turbine*, nyaya za umeme wenye msongo mkubwa hadi za matumizi ya majumbani, *transforma*, taa, *switches* na vifaa vinginevyo vya umeme. Kwa upande wa eneo la usambazaji, Algeria imefanikiwa kufikisha umeme kwa watumiaji kwa asilimia 99, ikiwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa megawatt 28,000. Aidha, uzalishaji wa vifaa na mahitaji mengine yanayohusisha usafirishaji na usambazaji wa umeme, nchi hiyo inajitosheleza kwa uzalishaji wa ndani kwa takriban asilimia 90.

 

Kupitia ziara hiyo, Mhe. Balozi alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Mkugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Djilani Kobibi Bachir ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Kongani ya Viwanda vya Umeme (CIEL). Mkurugenzi huyo, alieleza kuwa CIEL imepewa maelekezo mahsusi na Rais wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune kuhusu kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika kutafua suluhu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosheleza maendeleo ya bara hili.

 

Bw. Djilani alisisitiza kuwa miongoni mwa changamoto za uzalishaji zinazokabili bara hili ni uzalishaji mdogo kutokana na masharika ya umeme barani Afrika kujikita zaidi kwenye uzalishaji wa umeme kwa ajili ya matumizi ya majumbani ambayo hayazidi masaa 5 kwa siku. Hivyo, kuna haja ya kuimarisha uzalishaji kwa ajili ya ukuaji wa viwanda na uchumi ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto ya upotevu wa umeme inayosababishwa na miundombinu na matumizi ya teknolojia ya zamani.

 

Vilevile, Bw. Djilani aliweka wazi utayari wa CIEL kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kwa ajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na mamlaka husika juu ya maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano katika sekta ya umeme. Aliongeza kuwa GISB ipo tayari kuwekeza Tanzania iwapo itahakikishiwa upatikanaji wa malighafi muhimu hasa *aluminium, copper na bauxite*.

 

Kwa upande wake, Mhe. Balozi, alieleza kuwa kwa sasa uzalishaji wa umeme nchini Tanzania ni wastani wa Megawatt 4,000 ambapo mpango wa serikali ni kufikia megawatt 10,000 ifikapo mwaka 2030. Alieleza kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme kama vile maji, upepo, jua, joto ardhi na gesi asilia.

 

Hivyo basi, kutokana na uhusiano wa kirafiki, wa kihistoria na wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili, Tanzania imefungua milango na ipo tayari kushirikiana na Algeria kwenye uzalishaji wa umeme, usafirishaji, usambazaji pamoja na mafunzo ili kufikia malengo ya kuzalisha megawatt 10,000.

 

Mbali na mazungumzo hayo, Mhe. Balozi alipata nafasi ya kutembelea viwanda vya GISB Electric ikihusisha uzalishaji wa nyaya za umeme za aina mbalimbali, jenerata, switch, sockets, taa za barabarani na majumbani pamoja na maabara za kisasa kwa ajili ya kupima ubora na viwango vya bidhaa zinazozalishwa na GISB Electric.

 

Kampuni ya GISB Electric iliyoanzishwa mwaka 1965 ina ukubwa wa eneo la mita za mraba 130,000 na imeatoa Zaidi ya ajira 1,200 za moja kwa moja. Kampuni hiyo, imekuwa ikisafirisha bidhaa mbalimbali za umeme kwenye nchi za Ethiopia, Sudan, Mauritania, Senegal, Mali, Guinee n.k. Kadhalika, bidhaa zinazozalishwa na GISB Electric vimepata ithibati za viwango na ubora kutoka mamlaka za ndani na Ulaya.

 

Kufuatia Mazungumzo hayo, Mhe. Balozi alimuahidi Bw. Djilani kuhusu kuratibu ziara ya kikazi ya ujumbe wa GISB Electric nchini Tanzania mapema kati ya Desemba 2025 na Januari 2026 ili kuwezesha ujumbe huo kukutana na kufanya mazungumzo na Mamlaka za Tanzania kwa lengo la kuangazia maeneo ya kipaumbele ambayo Tanzania ingependa kupata msaada na uzoefu wa Algeria katika sekta ya umeme pamoja na uwezekanao wa kutekeleza miradi ya pamoja.