Leo tarehe 9 Aprili 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai amefanya mazungumzo na Bw. Soufian Mwakilishi wa Taasisi ya Serikali ya Kuandaa Maonesho na Kuhamasisha Mauzo ya Nje (SAFEX) katika Ofisi za Ubalozi jijini Algiers.
Kupitia kikao hicho, Bw. Soufian alimfahamisha Mhe. Balozi kuwa Taasisi ya SAFEX imejipanga kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam DITF49 na tayari wapo katika hatua za awali za maandalizi ambapo zaidi ya kampuni 30 za Algeria zinatarajiwa kushiriki katika Maonesho hayo.
Kwa upande wake Mhe. Balozi amemhakikisha Bw. Soufian kuwa Ubalozi upo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa ushiriki wa Algeria unafanikiwa na unafungua milango ya biashara kati ya nchi mbili.
Sambamba na hilo Mhe. Balozi ameitaka Taasisi ya SAFEX kuufahamisha Ubalozi kuhusu orodha ya kampuni zitakazoshiriki na ukubwa wa eneo watakalohitaji ili Ubalozi kufanya mawasiliano na Taasisi husika  nchini Tanzania kwa ajili ya uratibu na kuhakikisha kuwa suala lao linakwenda sawa.