Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai amewataka wadau wa utalii wa Algeria kuendelea kuongeza kasi ya kupeleka watalii nchini Tanzania ili kupata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kama vile fukwe za bahari, mbuga za wanyama pamoja na mlima Kilimanjaro.

Mhe. Balozi ameyasema hayo mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Utalii na Sanaa wa Algeria, Mhe. Houria Maddahi aliyetembelea Banda la Tanzania wakati wa uzinduzi wa Manesho ya Kimataifa ya Utalii nchini Algeria (SITEF 24) yaliyofanyika jijini Algiers katika viwanja vya maonesho vya SAFEX kuanzia tarehe 12 hadi 15 July 2025.

Aidha, Washiriki wa Maonesho hayo kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Mbuga za Wanyama Tanzania (TANAPA) pamoja na Kampuni ya Utalii ya Rough and Dusty ya Jijini Arusha walitumia jukwaa hilo kunadi Utalii wa Tanzania pamoja na kuwakaribisha wa Algeria kuwekeza nchini Tanzania katika sekta ya Utalii.

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Ujumbe wa TANAPA pamoja na Meneja wa Kampuni ya Utalii ya Rough and Dusty katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers na kuwapongeza kwa hatua muhimu ya kuja kutangaza utalii wa Tanzania nchini Algeria na kuunga mkono juhudi za Ubalozi. Aidha, kutokana na umuhimu wa soko la Algeria amewashauri kujipanga zaidi kushiriki tena Maonesho mbalimbali ya Utalii nchini Algeria ili kuweza kuzitangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Pamoja na mwitikio mkubwa wa Algeria kutaka kutembelea Tanzania bado watalii wa Algeria wanasumbuliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa usafiri wa moja kwa moja. Ubalozi unaendelea kushirikiana kwa karibu na Mamlaka husika nchini Algeria kuzishawishi kuanzisha safari za anga za moja kwa moja kati ya Tanzania na Algeria ili kuchochea zaidi utalii na shughuli nyingine za biashara na uwekezaji kati ya mataifa haya.