Tarehe 08 Aprili 2025, Mhe. Iman Njalikai, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Algeria amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Aminou Malam Manzo, Balozi wa Jamhuri ya Niger nchini Algeria katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo jijini Algiers.
Mhe. Balozi Njalikai alitumia fursa hiyo kumfahamisha mwenyeji wake kuhusu ziara ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Niger akiwa Mjumbe Maalumu wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mheshimiwa Jenerali Abdourahmane Tchiani, Rais wa Niger.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Balozi alieleza pia kuhusu uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Jamhuri ya Niger sasa iwakilishwe kutokea Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers.
Kwa upande wake Balozi Aminou amemhakikishia Mhe. Balozi Njalikai ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo yake ya uwakilishi ili kuimarisha ushirikiano mwema uliopo katika ya nchi hizi mbili.
Kwa pamoja, viongozi hao wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wa uwili na kuendeleza umoja na mshikamano wa Afrika ili kufaidika na fursa za mbalimbali za kikanda kupitia Mpango wa Soko huria la Afrika.

