Februari 4, 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Mbolea ya Sorfert, Bw. Maged El Tobgy makao makuu ya Kampuni hiyo jijini Oran.
Katika kikao hicho, Mhe. Balozi alielezea uhitaji wa mbolea nchini Tanzania katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo na kuangalia uwezekano wa kampuni hiyo kushirikiana na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuipatia mbolea Tanzania.
Pamoja na mambo mengine. Mhe. Balozi alieleza kuwa mahitaji ya mbolea nchini yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mikakati ya Serikali ya kusaidia wakulima ikiwemo kuboresha miundombinu na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji.
Aidha, kutokana na uhitaji mkubwa wa mbolea kwa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na uwepo gesi asilia, Mhe. Balozi ameiomba Sorfert kufikiria kuwekeza Kiwanda cha Mbolea nchini Tanzania.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa kampuni ya Sorfert, Bw. Maged pamoja na timu yake ya menejimenti ya Kampuni hiyo wameeleza utayari wa kushirikiana na Tanzania na kumhakikishia Balozi Njalikai kulifanyia kazi ombi la Tanzania kwa wakati.


