Tarehe 23 Julai, 2025 Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alimpokea Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis CHALAMILLA katika ofisi za Ubalozi Jijini Algiers.
Mkurugenzi huyo aliwasili nchini Algeria tarehe 19 Julai kwa ajili ya kuhudhururia Mkutano Mkuu wa 7 Shirikisho la Mamlaka za Kupambana na Rushwa Afrika - AAACA uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa CIC jijini Algiers.
Katika ziara yake Ubalozini, Mkurugenzi Mkuu alipokelewa na Mhe. Balozi Njalikai na Maafisa Ubalozi na kupata fursa ya kupokea Taarifa fupi ya shughuli za Ubalozi na maendeleo ya Ubalozi kwa upande wa Algeria ikiwemo kuchagiza zaidi ushirikiano katika eneo la diplomasia ya uchumi.
Mhe. Balozi Njalikai alisisitiza kuwa Algeria ni rafiki wa dhati wa Tanzania katika vipindi vyote. Aidha, nchi hiyo imepiga hatua kubwa za maendeleo ya kichumi barani Afrika na hivyo, kutoa fursa mihimu kwa Tanzania kujifunza na kushirikiana kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali hasa ya kiuchumi.
Mhe. Balozi alipongeza ziara za viongozi na watendaji wa Tanzania kushiriki katika majukwaa mbalimbali ya ushirikiano wa uwili, kikanda na Kimataifa yanayofanyika nchini Algeria ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alitumia nafasi hiyo kuushukuru Ubalozi kwa mapokezi mazuri na kuomba Ubalozi kuendelea kutekeleza majukumu yake bila ya kuchoka na kuwa na imani kuwa Tanzania iko salama.
Aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 TAKUKURU imejipanga vema kudhibiti na kupambana na viashiria vya rushwa kwa kutoa elimu kwa jamii na wanasiasa kwa lengo la kuwaasa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa maendeleo.





