Leo tarehe 06 Agosti 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, Mhe. Boualem Chebihi katika ofisi za Wizara hiyo jijini Algiers.

Wawili hao walijadili maendeleo ya utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano wa uwili kati ya Tanzania na Algeria hususan katika eneo la nishati, elimu pamoja na utalii. Kwa upande mwingine walipongeza  ziara za kisekta zilizofanywa na upande wa Tanzania nchini Algeria katika kipindi cha mwezi Juni na Julai 2025. Ziara hizo ni pamoja na ujumbe wa kampuni ya mbolea ya Tanzania, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na ujumbe wa TANAPA.

Sambamba na hilo, walijadili umuhimu wa kushiriki ipasavyo katika jukwaa la Kiuchumi la IATF2025  litakalofanyika jijini Algiers  mwezi Septemba 2025 ambalo linalenga kuimarisha na kuchagiza ushirikiano wa kibiashara miongoni mwa nchi za Afrika kupitia mkataba wa ushirikiano wa AfCFTA ambao Tanzania na Algeria ni wanachama.