Tarehe 20 Januari 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman S. Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama kikongwe, chenye ushawishi na uungwaji mkono mkubwa nchini Algeria cha Front Liberation Movement (FLN) Mhe. Abdelkrim Benmbarek katika ofisi za chama jijini Algiers.
Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati kuu ya FLN akiwemo Mwanamapinduzi Bw. Mourad Alamoudi, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mshauri wa Katibu Mkuu Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa ambaye alishiriki harakati mbalimbali za ukombozi wa Bara la Afrika nchini Tanzania.
Pamoja na mambo mengine viongozi hao walijadili umuhimu wa kuhuisha uhusiano na urafiki wa kihistoria na wa muda mrefu kati ya Chama hicho na Chama cha Mapinduzi. Kadjalika, waliangazia masuala mengine ya ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Tanzania na Algeria kupitia Chama cha FLN na Chama cha Mapinduzi na kuona haja ya kuongeza nguvu ya ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kama vile nishati, elimu, kilimo na uzalishaji wa dawa ili kukabiliana na changamoto za sasa kikanda na kimataifa.
kwa upande mwingine viongozi hao walijadili mpango wa kuhuisha uhusiano na ushirikisno wenye misingi imara wa vyama hivyo kupitia kubadilishana ziara kwa viongozi waandamizi wa chama kwa lengo la kubadilishana uzoefu na taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa kikanda na Kimataifa na kudumisha udugu wa kihistoria pamoja na kujenga umoja na mshikamano imara katika kulinda na kutetea maslahi ya wananchi wa nchi hizo mbili.




