Dkt. Suleiman Serera, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 6 Septemba 2025 alifanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki kwenye Maonesho ya Biashara Afrika {IATF2025} yanayofanyika Jijini Algiers kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba 2025. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za Ubalozi zilizopo jijini Algiers.
Dkt. Serera, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye maonesho hayo ya IATF2025 uliyoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Viwanda iliyopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ujumbe wa Tanzania unajumuisha taasisi mbalimbali za serikai pamoja na taasisi binafasi kama vile TIC, ZIPA, TMDA, MSD, NEMC, CRDB na TASAC.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIPA Mhe. Balozi Omar Yussuf Mzee na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Bw. Mussa Hamza Mandia, walipata fursa ya kutembelea Banda la Tanzania katika viwanja vya maonesho vya Safex pamoja na kushiriki matukio mbalimbali yenye lengo la kuhamasisha uwekezaji na biashara. Lengo kuu la ushiriki ni kuchochea ushirikiano wa biashara kikanda kati ya nchi za Afrika na kushawishi wafanyabiashara na wawekezaji wa nje kuitumia Tanzania kama nchi ya kimkakati kikanda kibiashara na uwekezaji.
Mhe. Naibu Katibu Mkuu, ameupongeza na kuushukuru Ubalozi kwa ushirikiano wa karibu na ujumbe wa Tanzania wa IATF2025. Aidha, amewataka washiriki wote kutoka Tanzania kuwa kitu kimoja bila ya kujali Taasisi wanazotoka na kufanya kazi kwa karibu na Ubalozi. Katika hatua nyingine, Mhe. Naibu Katibu Mkuu amewataka wawakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na TanTrade kuratibu na kusimamia ipasavyo ushiriki wa Tanzania ili kuwa na matokeo yenye tija pamoja na kuwa na mpango mzuri wa ufuatiliaji baada ya maonesho.
Awali, Mhe. Naibu Katibu Mkuu pamoja na Mhe. Balozi walishiriki katika ufunguzi rasmi wa maonesho hayo ya IATF2025 uliofanywa na Mhe. Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria tarehe 4 Septemba 2025. Wakuu wengine wa nchi kutoka Msumbiji, Tunisia, Lybia, Mauritania na Chad pia walishiriki ufunguzi huo. Kadhalika, Makamu wa Rais wa Kenya na Namibia na Waziri Mkuu wa Burundi nao walikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri walioshiriki sherehe za ufunguzi.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Njalikai alieleza kuhusu uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Algeria na uwepo wa fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji katikati sekta za afya, kilimo, nishati, fedha, uchumi wa buluu, miundumbinu pamoja na biashara sanjari na juhudi zinazofanywa na Ubalozi katika kusimamia sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa ujumbe wa Tanzania wa IATF2025 kuutumia Ubalozi kupata taarifa sahihi na muhimu kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini Algeria pamoja na kukutanishwa na mamlaka na wadau husika ili kutengeneza misingi imara na uaminifu ya biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili.







