Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria kwa kushirikiana na Wakala wa Ukuzaji Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) umeandaa Kongamano la biashara, uwekezaji na utalii jijini Algiers tarehe 14 Mei 2025.   Lengo la kongamano hilo ni kutangaza fursa za biashara na uwekezaji  katika sekta ya viwanda, dawa, madini, uchakataji wa bidhaa za chakula, utalii, nishati na uchumi wa buluu.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Mhe. Balozi Iman Njalikai na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Mkurugenzi wa Ofisi ya Waziri wa Nchi, Nishati na Madini, Mwakilishi wa Wizara ya Uchumi wa Maarifa, Startsup na Kampuni Changa, Kituo cha Maendeleo na Uwekezaji cha Waarabu wa Afrika (CAAID), Shirika la Serikali Tasdiir, Taasisi ya Maendeleo ya Kiuchumi (ONDE) wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali, mashirika ya ndege pamoja na mawakala wa Utalii.

Katika kufungua kongamano hilo, Mhe. Balozi Njalikai alieleza uhusiano imara uliyopo kati ya Tanzania na Algeria na kusisitiza umuhimu wa kutumuia uhusiano huo  kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi hususan katika sekta ya nishati, kilimo, viwanda vya madawa, ufugaji wa mazao ya bahari, maeneo ambayo Algeria ina uzoefu wa muda mrefu na imekuwa ikifanya vizuri.

Aidha, Mhe. Balozi alieleza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji pamoja na sera rafiki za kikodi kwa wawekezaji, juhudi za Serikali za kuimarisha miundo mbinu ya Barabara na reli na kuunganisha nchi jirani, soko la uhakika la ndani pamoja na masoko ya kikanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, utulivu na amani ya nchi kisiasa na ukuaji imara wa uchumi ni mambo yanayoifanya Tanzania kuwa sehemu sahihi na kimbilio la uwekezaji na biashara.

Viongozi mbalimbali wa Serikali walipata nafasi ya kuchangia na kuwahamasisha wawekezaji na Wafanyabiashara wa Algeria kuitumia Tanzania kama lango la biashara kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki pamoja na kushiriki ipasavyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu SABASABA yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025.