Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria umeadhimisha miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili 2025 Jijini Algiers.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Waziri wa Nishati, Madini na Nishati Jadidifu, Mhe. Mohamad Arkab, Wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, wawakilishi kutoka Wizara ya Ulinzi ya Algeria, Waheshimiwa Mabalozi, wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini Algeria, Waambata Jeshi, Diaspora pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.
Aidha, kupitia hotuba yake ya kuadhimisha siku hiyo, Mhe. Balozi Iman Njalikai aliwasilisha salamu za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mheshimiwa Rais Tebboune wa Algeria na watu wa Algeria na wageni waalikwa.
Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio mbalimbali ya muungano kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwemo Tanzania kufikia katika nchi ya uchumi wa wakati, maendeleo ya miradi ya miundombinu kama vile mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma uliozinduliwa rasmi mwaka 2024 pamoja na maendeleo ya nishati, mradi wa bwawa la umeme la Mwalimu nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawat 2,115 na kuungnishwa na mkongo wa Taifa.
Kadhalika, Mhe. Balozi alieleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Algeria na Tanzania na makubaliano ya ushirikiano yaliyopo kati ya nchi mbili yanayohusisha sekta ya nishati, elimu biashara, utamaduni na kuwataka wafanyabiashara wa nchi zote mbili kutumia fursa hiyo kufaidika na fursa zilizopo kutoka kila upande.
kwa upande mwingine, Mhe. Balozi ameeleza msimamo thabiti wa Tanzania wa kuendelea kushirikiana na washirika wake kikanda na kimataifa katika kukabiliana na changamoto za ugaidi, mabadiliko ya tabia ya nchi, dawa za kulevya na biashara ya watu.
Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi alitumia nafasi hiyo kuziomba nchi rafiki na washirika wa Tanzania kuunga mkono juhudi za Tanzania na kuumunga Mkono Prof. Mohamed Yakub Janabi katika nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ili kuleta mabadiliko ya Sekta ya Afya Barani Afrika.







