Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai ameungana Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuadhimisha siku ya Jumuiya tarehe 17 Agosti 2025 jijini Algiers.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mabalozi mbalimbali wa nchi rafiki, Viongozi wa Serikali pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini Algeria.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Umoja wa Mabalozi wa Nchi za SADC, Balozi wa Zimbabwe Mhe. Ntonga alieleza kuhusu fursa za kiuchumi na biashara zilizopo kwenye soko la SADC na kuwataka Wafanyabiashara wa Algeria kuona namna ya kulitumia soko hilo ili kujenga ushirikiano imara wa kiuchumi.
Naye mgeni rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Mhe. Selma Bakhta Mansouri alieleze juu ya umuhimu wa Jumuiya ya SADC katika kuchagiza Maendeleo ya Uchumi, Ulinzi na Usalama kikanda na Kimataifa.
Mhe. Mansour alisisitiza kuwa Algeria itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya SADC katika masuala mazima ya Maendeleo, ulinzi na usalama.
Aidha, Mhe. Mansour alitoa wito kwa nchi za SADC kushiriki ipasavyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Afrika (IATF2025) yatakayofanyika jijini Algiers kuanzia tarehe 4 hadi 9 Septemba 2025.
Hafla hiyo ilimalizika kwa dhifa ya mapishi mbalimbali ya chakula cha kiafrika kilichoandaliwa na Balozi wanachama wa nchi za SADC waliopo nchini Algeria.


