Tarehe 20 Oktoba 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alipokea mwaliko kutoka kwa Bi. Ghoufrane Bourtal Zarat, Meneja wa Mipango wa Kampuni ya EURI Elevent Event waandaaji na waratibu wa Maonesho ya Kimataifa ya Ujenzi (BATIMEX) yanayofanyika  mwezi Januari ya kila mwaka jijni Annaba.

Kupitia mwaliko huo, Kampuni ya EURl Eleven Event imeziomba Taasisi na mashirika ya ujenzi nchini Tanzania pamoja Wasanifu majengo kushiriki Maonesho ya BATIMEX yatakayofanyika mwakani kuanzia tarehe 28 hadi 31 Januari, 2026 Jijini Annaba katika hoteli ya Sheraton na kulitumia jukwaa hilo kutengeneza fursa mbalimbali za ushirikiano ambapo zaidi ya kampuni 150 zitashiriki kwenye maonesho hayo, zikiwemo kampuni za uzalishaji wa vifaa vya ujenzi pamoja na kampuni za ujenzi (real estates developers).

Kwa upande wake Mhe. Balozi mbali na shukurani, alimhakikishia Bi. Ghoufrane kuwa Ubalozi utaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha kuwa mwaliko huo unafika kwa taasisi husika mapema kwa ajili ya kujiandaa kushirki ipasavyo. Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alishauri waratibu wa Maonesho hayo kuona namna bora ya kuratibu maonesho na ziara za viwandani kwa washiriki kutoka nje ya Algeria ili kupata nafasi ya kuona uzalishaji na miradi ya ujenzi inayoendelea nchini Algeria ili kupata taswira sahihi na kuona fursa zilizopo.