Tarehe 26 Sepetemba 2025, Mhe. Iman Njalikai, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Boualem Chebihi, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Algiers.
Lengo la mazungumzo hayo, lilikuwa ni kuangazia hali ya utekelezaji wa mikataba na makubaliano mbalimbali ya ushirikiano wa uwili kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria. Kadhalika, wawili hao walikubaliana kuongeza kasi ya ufuatiliaji kuhusu ukamilishaji wa rasimu mbalimbali za makubaliano ambazo bado kusainiwa.
Eneo lingine lililopewa kipaumbele ni umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika agenda mbalimbali zinazohusu umajumui na mtangamano wa Afrika kwenye Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kimataifa na Kanda hususan katika kupaza sauti za utetezi wa haki za wanyonge.
Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi Njalikai alitumia fursa hiyo kuwasilisha shukurani za dhati na pongezi za kipekee kwa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Algeria kwa uratibu mzuri wa viwango vya juu kabisa wa maonensho ya IATF2025 yaliyofanyika jijini Algiers kuanzia tarehe 04 - 10 Septemba 2025 ambapo Tanzania ilishiriki kikamilifu.
