Tarehe 14 Julai 2025, Mhe. Balozi Iman Njalikai alimpokea Mhe. Geophrey Mizengo Pinda (MB), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Houari Boumedienne jijini Algiers. Mhe. Naibu Waziri yupo ziarani nchini Algeria kwa ajili ya kuhudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa Shelter Afrique unaofanyika jijini Algiers kuanzia tarehe 15 hadi 17 Julai 2025 katika ukumbi wa Hotel ya El Aurassi.
Aidha, tarehe 16 Julai 2025, Mhe. Naibu Waziri alitembelea Ofisi za Ubalozi na kupata nafasi ya kuzungumza na Mhe. Balozi pamoja na Maafisa Ubalozi ikiwemo kupokea taarifa fupi ya kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ubalozi.
Kadhalika, katika sekta ya ardhi na makazi, Mhe. Balozi alisisitiza kuwa yapo mengi ya kujifunza kutoka Algeria hususan miradi ya ujenzi wa makazi ya wananchi inayosimamiwa na Serikali. Hivyo, alitoa wito kwa NHC na taasisi nyingine zinazotekeleza miradi ya makazi kwenye eneo hilo kuona namna nzuri ya kufanya kazi na wenzao wa Algeria.
Kwa upande wake, Mhe. Naibu Waziri ameutaka Ubalozi kusimamia na kutetea maslahi ya nchi bila ya kuchoka na kuzishauri mamlaka juu ya fursa zilizopo katika eneo la uwakilishi ili kujenga ushirikiano imara na wenye tija.


