Tarehe 05 Oktoba 2025, Mhe. Balozi Njalikai katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa  Kampuni ya "Cultivate Africa", Dkt. Sharon Reyes mtaalamu wa kilimo  kutoka Netherland ambaye amefungua ofisi zake nchini Algeria.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya kampuni ya "Cultivate Africa" kununua  mazao ya kilimo kwa ajili ya soko la Algeria ambalo linaagiza bidhaa nyingi za kilimo kutoka Amerika ya Kusini na Asia.

Kwa upande wake Dkt. Sharon aliweka wazi kuwa dhamira yake ya kutaka kufanya biashara na Tanzania inatokana ubora wa bidhaa za kilimo za Tanzania. Kupitia ziara zake nchini Tanzania pamoja na kushiriki kwenye baadhi ya miradi ya kilimo, Dkt. Sharon amevutiwa zaidi na ubora wa viungo kutoka Tanzania hususan kama vile karafuu, tangawizi pamoja na pilipili mtama.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Njalikai amemhakikishia Dkt. Sharon utayari wa Ubalozi kushirikiana naye katika mpango wake wa uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania. Aidha, Ubalozi upo tayari kumtambulisha katika mamlaka husika za biashara na kilimo nchini Tanzania ili kuhakikisha kuwa anafanya kazi na Taasisi stahiki.

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alikaribisha mpango wa Dkt. Sharon kuandaa ziara ya  wafanyabiashara wa Algeria pamoja na diaspora wa Afrika wenye nia ya kuwekeza barani Afrika kutembelea Tanzania kwa ajili ya kungalia fursa za biashara na uwekezaji Januari 2026.