Tarehe 19 Aprili 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Uhuishaji Uchumi nchini Algeria (CREA), Mhe. Kamal Moula, katika ofisi za CREA zilizopo jijini Algiers.

CREA ni Baraza  muhimu katika kujenga ushirikiano wa kiuchumi kati ya  Algeria na Tanzania. Taasisi hii  ilianzishwa mwaka 2022 ikiwa na jukumu la kuziweka pamoja taasisi za kiuchumi za umma na binafsi kwa ajili ya kujenga uchumi imara  wa viwanda.

Kupitia kikao hicho, viongozi hao walijadili fursa mbalimbali za biashara zilizopo Algeria ambazo Tanzania  inaweza kufaidika kama vile  uzalishaji wa dawa za binadamu, uongezaji thamani wa bidhaa hasa za kilimo, vifaa vya umeme pamoja na vifaa vya ujenzi.

Kadhalika, Tanzania inayo fursa kubwa ya kuuza mazao ya kilimo ikiwemo kahawa, korosho, mchele pamoja na viungo. Haya ni jumla ya mazao ambayo Algeria inategemea kwa kiasi kikubwa uagizaji kutoka bara la Asia na Afrika  na Amerika ya kusini.

Sambamba na hilo, viongozi hao walikubaliana kuanzisha ushirikiano  kati ya CREA na Chemba ya Biashara na Viwanda na Kilimo ya Tanzania TCCIA pamoja na Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.