Tarehe 07 Mei 2025, Mhe. Balozi Iman Njalikai amekutana na kufanya mazungumzo na Dr. Amir Ben Ammar pamoja na Dr. Mussa Sissoko katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers.
Wadau hao wa sekta ya Afya walimueleza Mhe. Balozi kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Afya unaolenga kuwakutanisha Wadau muhimu wa Afya Barani Afrika utakaofanyika tarehe 13 Julai 2025 katika Hoteli ya Sheraton Jijini Annaba nchini Algeria.
Lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau muhimu wa Afya Barani Afrika na kuwa na mtandao wa pamoja kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kwenye kada mbalimbali za afya ikiwemo utoaji huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, maradhi ya akina mama nk.
Kadhalika, kuwajengea uwezo madaktari kupitia mafunzo ya muda mfupi yatakayotolewa na wataalamu na Taasisi za Algeria kupitia mpango endelevu wa ushirikiano pamoja na kuandaa ziara za timu za madaktari wa Algeria kutembelea Tanzania.
kwa upande wake Mhe. Balozi amewapongeza wadau hao kwa kuja na mpango wa kuendeleza na kukuza sekta ya Afya Barani Afrika. Aidha, Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kuwaeleza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Rufaa kila Mkoa, Hospitali za Wilaya na Zahanati katika ngazi za Vijiji.
Mhe. Balozi aliongeza kuwa Tanzania ni Kituo kikubwa cha Utalii tiba kwa Afrika Mashariki na inapokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za jirani kama vile, Msumbuji, DRC, Burundi, Rwanda, Comoro nk. Moja katika eneo ambalo Tanzania inafanya vizuri ni pamoja na operesheni za magonjwa ya moyo zinazofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete.
Kupitia fursa ya Kongamano hilo na umuhimu wake kwa Tanzania, Mhe. Balozi amewataka waandaji hao kutoa mialiko mapema kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kuwasilisha kwa Taasisi husika na kuona uwekezano wa ushiriki wa Taasisi za Tanzania.
