Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria umeshiriki katika Jukwaa la 11 la Afrika la Biashara na Uwekezaji (AFIC11) lililoandaliwa na Kituo cha Waarabu wa Afrika cha Uwekezaji na Maendeleo lililofanyika katika Hoteli ya Sheraton Jijini Algiers tarehe 10 na 11 Mei 2025.
Jukwaa hilo lilifunguliwa rasmi na Waziri wa Uhamasishaji wa Biashara za Nje wa Serikali ya Algeria, Mhe. Kamel Rezig na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Kiserikali akiwemo Waziri wa Kazi, Mhe. Lakdhar Rakhroukh, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uwekezaji Algeria, Mhe. Omar Rekkache, Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Wizara ya Nishati. Wengine walioshiriki ni Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika, Taasisi mbalimbali za Umoja wa Afrika kama vile AfCFTA, Afreximbank, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Waheshimiwa Mabalozi, Mamlaka za Uwekezaji, Wawekezaji na Wafanyibiashara pamoja na wadau muhimu wa kiuchumi barani Afrika.
Kupitia hotuba yake Mhe. Balozi Iman Njalikai iliyosomwa na Mwambata Ubalozi Bw. Suleiman Mussa, Mhe. Balozi ametowa wito kwa nchi za Afrika kushikamana na kujenga ushirikiano imara kiuchumi kupitia fursa zilizopo kwenye soko la ukanda huru wa Afrika. Aidha, Mhe. Balozi alieleza kuwa mauzo ya biashara kati ya nchi za Afrika bado yako chini na yanategemea kwa kiasi kikubwa uuzaji wa malighafi ambazo bado hazijachakatwa. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuongeza nguvu kwenye eneo la kuongeza thamani kwenye bidhaa.
Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi alisisitiza kuwa Afrika inalo soko kubwa la watu Bilioni 1.5 linalozidi thamani ya Dola za Marekani trilioni 4. Hivyo, alitoa wito kwa kuwaomba washiriki wa jukwaa hilo kutumia fursa hiyo kuwekeza na kufanyabiashara na Tanzania, nchi ya kimkakati kijiografia yenye masoko muhimu ya kikanda, soko la Afrika Mashariki na Soko la nchi za Kusini mwa Afrika.
Kwa uchache, Mhe. Balozi aliainisha maeneo ya kipaumbele na kimkakati kwa uwekezaji nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii, uchukuzi wa bahari, uvuvi na ufugaji wa mazao ya bahari, uchakataji wa mazao ya kilimo, viwanda, mafuta na gesi, ujenzi, IT, fedha na mengineyo.
Aidha, Mhe. Balozi aliweka wazi utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuendelea kufanya kazi na Wadau wote kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na kuwataka wadau mbalimbali kutembelea Tanzania, Ardhi ya Mlima Kilimanjaro, Zanzibar na Serengeti.


