Tarehe 7 Septemba 2025, Balozi wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo kutembelea kiwanda cha Dawa za Binadamu na Vifaa Tiba cha Biopharm kilichopo jijini Algiers.

 

Dkt. Fimbo ameongoza ujumbe wa IATF2025 kutoka Wizara ya Afya akiwa na mwakilishi wa wizara, wajumbe wa TMDA pamoja na MSD. Lengo kuu ni kuwashawishi wawekezaji wa Viwanda vya Dawa hususan kutoka Algeria kuwekeza katika sekta ya dawa nchini Tanzania na kusajili dawa zao katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) pamoja na kuwahakikishia soko la bidhaa zao kupitia Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).

 

Katika kufanikisha azma hiyo, Mhe. Balozi pamoja na Ujumbe wa Wizara ya Afya ulitembelea Kiwanda cha wazawa cha Dawa za binadamu na vifaa tiba cha Biopharm na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kiwanda hicho akiwemo Mtendaji Mkuu. Wengine walojumuika naye ni Mkurugenzi wa Mauzo, Bi. Mouna Boukhelfa, Mkurugenzi wa Uzalishaji, Bw. Ayadi Elghani na Mkurugenzi wa maendeleo Bw. Abelhalim Benmerad.

 

Kupitia mkutano huo, Ujumbe wa Wizara ya Afya ulipata fursa ya kuona historia ya kiwanda hicho, maendeleo ya uzalishaji wa dawa na utanuzi wa kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za kansa na uzalishaji wa homoni.

 

Biopharm ni moja ya viwanda vya wazawa vinavyofanya vizuri kwenye uzalishaji wa dawa katika soko la ndani na nje ya nchi. Kwa sasa Biopharm ni wazalishaji na wasambazaji wa Dawa katika nchi za Afrika Magharibi kama vile Mauritania, Senegal, Ivory Coast, Cameroon nk.

 

Ujumbe wa Wizara ya Afya kupitia kiongozi wake Dkt. Fimbo ulipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ya kitaalamu kuhusu ubora na viwango vya dawa zinazozalishwa kiwandani hapo na kutembelea Mtambo wa Uzalishaji wa vidonge. Sambamba na hilo, Dkt. Fimbo alitumia fursa hiyo kueleza utaratibu wa usajili wa dawa Tanzania, motisha  zinazotolewa na Serikali kwa wazalishaji wa ndani na kuwakaribisha Biopharm kusajili dawa zao Tanzania na kuwahikikishia kuwapa ushirikiano.

 

Kadhalika, Mwakilishi wa MSD Bw. Undule Korosso alieleza majukumu mbalimbali ya  MSD ikiwemo ununuzi, uhifadhi  na usambazaji wa dawa. Dawa zinazohitajika zaidi katika soko la Tanzania pamoja na vifaa Tiba pamoja na mpango wa MSD kujiimarisha kuwa na kiwanda chake ambacho kwa sasa ni kichanga.

 

Kwa upande wake Mhe. Balozi alitilia mkazo umuhimu wa Biopharm kusajili dawa zao Tanzania pamoja na kutoa fursa za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa kitanzania wanaosoma katika vyuo vikuu vya Algeria ili kupata uzoefu na kuwajengea uwezo.

 

Kwa upande wao Biopharm walieka wazi kuwa wanao mpango wa kusajili dawa zao Tanzania na tayari wanao uzoefu wa masoko ya nje. Kadhalika, wamelipokea ombi la Mhe. Balozi na kuwakaribisha wanafunzi wa Kitanzania kufanya mazoezi ya vitendo katika viwanda vyao.