*📌REA yapongezwa kwa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia*

*📌Tanzania, Algeria kuimarisha ushirikiano katika miradi ya umeme*

 

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Imani Njalikai ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa miradi ya umeme vijijini ambapo vijijini vyote nchini vimefikiwa kuwa na nishati ya umeme.

Hayo yamebainishwa na Balozi Mhe, Njalikai wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na Menejimenti ya REA nchini humo iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na nchi hiyo katika sekta ya nishati sambamba na kuanisha maeneo ya kimkakati ili kuwavutia wawekezaji katika sekta ya nishati.

Balozi Njalikai ameitaka REB na REA kutumia fursa ya ziara hiyo nchini Algeria ya kujifunza namna bora ya kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme hususan katika maeneo ya vijijini na maeneo ya pembezoni mwa miji ili kuwaletea maendeleo Watanzania katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema ziara hiyo nchini humo imekuwa na mafanikio hususan katika kuifanya miradi ya sekta ya nishati inakuwa  endelevu kwa manufaa ya taifa kwa jumla.

"Mafunzo tuliyoyapata hapa toka tumefika ikiwemo namna ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini nchini Algeria sambamba na kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali watendaji wa sekta ili kuweza kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi, " Amesema Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Kingu.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy ameushukuru ubalozi kwa mapokezi mazuri yaliyolenga kujifunza fursa mbalimbali katika sekta ya nishati, namna ya kuwajengea uwezo watumishi na kujitegemea katika ujuzi na vifaa.

"Kupitia mafunzo hayo tutaimarisha ushirikiano na wenzetu wa Algeria katika sekta ya nishati ili tutumie fursa hii muhimu ambayo itakua msaada mkubwa katika kuongeza ufanisi katika mazingira yetu nchini, " Amesema Mha. Saidy.

Ziara hiyo nchini REB na Watendaji wa REA nchini Algeria imelenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hiyo na Tanzania hususan katika maeneo ya kimkakati katika nishati pamoja na kubainisha maeneo ya kipaumbele yanayopaswa kupewa nguvu katika ushirikiano huo.