Mhe. Balozi Iman Njalikai tarehe 30 Juni 2025 alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania  (TFC) Bw. Samuel A. Mshote ambaye yupo kwenye ziara ya kikazi nchini Algeria. Kikao hicho kilifanyika katika ofisi za  Ubalozi jijini Algiers.

Kwa upande wake Mhe. Balozi amemueleza Mkurugenzi Mkuu kuwa Algeria na Tanzania ni marafiki wa kihistoria na huu ni wakati sahihi kwa nchi zote mbili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara.

Aidha, aliongeza kuwa TFC inayo fursa kubwa ya kuimarisha ushirikiano  na wenzao wa Algeria kwenye eneo la uzalishaji wa  mbolea. Mhe. Balozi alisisitiza kuwa Algeria ni kati ya nchi zenye uzoefu na uwezo mkubwa ambazo zinafanya vizuri katika uzalishaji wa mbolea.

Kadhalika, kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu alimthibitishia Mhe. Balozi kuwa ziara yao ya kikazi nchini Algeria imeenda vizuri na yapo mengi ya kujifunza kutoka Algeria.

Sambamba na hilo, TFC imemhakikishia Mhe. Balozi kuwa ipo tayari kufanya kazi kwa karibu na wenzao wa Algeria ili kufanikisha upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za mbolea kwa wakulima wa Tanzania.