Kupitia ushiriki wa Ujumbe wa Tanzania kwenye maonesho ya IATF2025 yanayoendelea nchini Algeria, Mhe. Balozi Iman Njalikai alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mhe. Wassim Kouidri, Waziri wa Viwanda vya Dawa wa Algeria katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo jijini Algiers.

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi aliambatana na ujumbe wa Wizara ya Afya ulioongozwa na Dkt. Adam Fimbo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamla ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), na kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pamoja na mwakilishi wa Wizara ya Afya. Kwa upande wake Mhe. Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Dawa Algeria (ANEP) na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Dawa cha Serikali (SAIDAL).

 

Kwa pamoja viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi za Umma kwenye eneo la Dawa upande wa MSD na SAIDAL na TMDA na ANEP sambamba na kutekeleza programu za pamoja zenye lengo la kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya.

 

Kupitia kikao hicho, ujumbe wa Tanzania ulipata nafasi kujifunza kuhusu sera za Algeria katika uwekezaji wa viwanda vya dawa ikiwemo vivutio na mikakati mingine yenye kusaidia uwekezaji na kukua kwa sekta nzima. Hadi sasa, Algeria ina jumla ya viwanda vya Dawa visivyopungua 200 ambavyo vinazalisha wastani wa takriban asilimia 83 ya mahitaji ya ndani. 

 

Kadhalika katika upande wa ubora, bei na viwango, Mhe. Waziri aliweka wazi kuwa viwanda vya Algeria vinakagukiwa kila mara na mamlaka husika na hawaruhusu dawa zisizo na viwango. Kadhalika, dawa zinazozalishwa ni za gharama  nafuu ikilinganishwa na nchi nyingi duniani.

 

Katika kufikia malengo ya ushirikiano wenye tija, ANEP wameshawasilisha rasimu ya Ushirikiano na TMDA. Vilevile, Kampuni ya Serikali ya Dawa SAIDAL wako tayari kuupokea ujumbe wa MSD Medipharm kwa ajili mazungumzo zaidi ya kibiashara na uwekezaji pamoja na kubadilishana uzoefu.