Leo tarehe 10 Januari 2025, Mhe. Balozi Iman Salum Njalikai amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara Ulaya, Mhe. Mohammad Amine Mohamade Bachir na Mkurugenzi Msaidizi wa Afrika, Mhe. Mohamad Youcef kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Mauritania, jijini Nouakchott nchini Mauritania.

Kupitia kikao hicho, Mhe. Balozi alimfahamisha Mkurugenzi kuwa lengo la ziara yake nchini Mauritania ni kuungana na Club ya Yanga ya Tanzania ambayo inacheza mchezo wake wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al hilal Omdurman ya Sudan mnamo tarehe 12 Januari 2025 katika uwanja wa Sheikha Ould boidiya jijini Nouakchott –Mauritania.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Balozi alimfahamisha Mkurugenzi huyo kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria kwa sasa ndio ambao utakuwa unawakilisha nchini Mauritania na mara baada ya taratibu kukamilika atawasilisha rasmi nakala na hati za uwakilishi.
Katika muktadha wa ushirikiano, viongozi hao walijadili fursa mbalimbali za ushirikiano kiuchumi kati ya nchi mbili ikiwemo kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya kilimo katika kukabiliana na changamato ya usalama wa chakula barani Afrika.

Mbali na masuala ya ushirikiano wa uwili, viongozi hao pia walitilia mkazo kuhusu ushirikiano wa kikanda hususan katika kujenga umoja na mshikamano wa Afrika.

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi wa huyo alimhakikishia Mhe. Balozi kuwa katika kipindi hiki cha uwenyekiti wa Umoja wa Afrika chini ya Mhe. Mohammed Ould Ghazouani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania wataendelea kutetea maslahi mapana ya Afrika kimataifa kupitia Umoja wa G7 na G20 na majukwaa mengine ya kikanda na kimataifa.

Sambamba na hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mauritania imelipokea kwa furaha shauri la uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwakilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyepo Jijini Algiers na kuahidi kutoa ushirikiano katika kujenga uhusiano imara kati ya Tanzania na Mauritania.