Tarehe 23 Aprili 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la umeme na gesi nchini Algeria (Sonelgas), Bw. Rachid Abdessemed katika ofisi za shirika hilo zilizopo jijini Algiers.

Kikao hicho kililenga kusukuma mbele ushirikiano wa nishati hususan umeme na gesi kati ya Tanzania na Algeria kupitia mikataba ya ushirikiano iliyosainiwa kati ya Sonelgas na TPDC na TANESCO mwezi Agosti mwaka 2023.

Kupitia kikao hicho, wawili hao walizungumzia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kwenye eneo la nishati kati ya nchi mbili na utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa mwaka 2023 wakati wa Mkutano Mkuu wa tano (5) Tume ya Kudumu ya Ushirikiano.

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi Njalikai alikumbushia mwaliko wa Taasisi ya REA kwa Sonelgas kutembelea Tanzania kati ya mwezi Julai hadi Septemba 2026 na kusisitiza umuhimu wa ziara hiyo kama hatua muhimu kwa Sonelgaz kupata nafasi ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya nishati ya REA.

Kwa upande mwingine, Kaimu Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgas alimhakikishia Mhe. Balozi kuwa Sonelgas itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote ya kipaumbele na wako tayari kupokea timu ya Tanzania kwa ajili ya mafunzo kama ambavyo wako tayari kuratibu ziara ya kutembelea Tanzania kwa ajili ya kukutana na REA, TANESCO na TPDC.