Tarehe 24 Septemba 2025, Mhe. Iman Njalikai, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria alifanya mazungumzo na Bw. Djilani Kobibi Bachir, Naibu Mwenyekiti wa Umoja wa Viwanda vya Uzalishaji wa Vifaa vya Umeme nchini Algeria (CIEL) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Umeme ya GISB. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers.
Kwa pamoja viongozi hao walijadili namna bora ya kuendeleza ushirikiano kwenye eneo la nishati hususan ya umeme na uwekezaji wa viwanda nchini Tanzania kwa kutumia uzoefu na utaalamu wa Algeria. Nchi hiyo, inajitosheleza kwa mahitaji ya umeme kwa asilimia zaidi ya 100. Hivi sasa, Algeria inazalisha Megawati takriban 28,000 ikilinganishwa na mahitaji ambayo ni chini ya gawati 20,000. Kadhalika, Algeria inajitegemea kwa takriban asilimia 100 katika uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme. Vivyo hivyo, asilimia 100 ya wataalamu wanaotumika ni wazawa (Waalgeria).
Aidha, Umoja wa viwanda vya uzalishaji wa umeme nchini Algeria umelenga kuanzisha uhusiano wa kimkakati na Tanzania kutokana na nafasi ya Tanzania kikanda, kijiografia na uwepo wa rasilimali na malighafi nyingi za viwandani kama vile chuma, makaa ya mawe na gesi ambazo zinaifanya Tanzania kuwa na hitajio kubwa la nishati ili kujiendeleza kiviwanda na kuwa na uzalishaji wa gharama nafuu ikiwemo pia kuhudumia maeneo ya jirani.
Kwa pamoja, uongozi wa umoja wa viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini Algeria wako tayari kwenda Tanzania kwa ajili ya ziara rasmi ya kikazi na kukutana na kufanya mazungumzo na mamlaka za Tanzania ili kuwa na makubaliano ya Mpango wa pamoja wa kimkakati wa kuendeleza nishati ya umeme nchini Tanzania.


