Tarehe 17 Machi 2025, Mhe. Balozi Iman Njalikai alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Abdelhaki Saihi, Waziri wa Afya wa Algeria katika Ofisi za Wizara hiyo jijini Algiers. Mhe. Balozi alitumia fursa hiyo kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Algeria katika kuendeleza sekta ya Afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya vya kisasa pamoja na utoaji huduma bora za matibabu.
Aidha, Mhe. Balozi aliweka wazi juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuimarisha sekta ya Afya ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya afya. Aliongeza kuwa nia ya Tanzania ni kuendelea kushirikiana na Algeria kwenye eneo hilo la Afya kupitia Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kwenye eneo hilo ambayo ipo upande wa Algeria kwa ajili ya mapendekezo zaidi. Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni mafunzo, kuendesha programu za pamoja na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande mwingine, wawili hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala kadhaa ya Kikanda na Kimataifa yenye mwelekeo wa afya.

