Tarehe 24 Agosti 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai amepokea na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) katika ofisi za Ubalozi jijini Algiers.

Ujumbe huo umeongozwa na Meneja wa Kanda Bw. Nteminyanda Kandoro na upo katika ziara ya kikazi nchini Algeria kwa  ajili ya kujifunza na kuangalia fursa mbalimbali za ushirikiano ili kuiwezesha TPDC kufanya kazi kwa weledi na ufanisi zaidi na kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya Serikali ya mwaka 2050.

Kwa upande wake Mhe. Balozi alikumbushia kuwa Algeria ni moja ya nchi zinazofanya vizuri katika eneo la nishati barani Afrika. Aidha, kupitia shirika lao la SONATRACH Algeria iliweza kushirikiana na Tanzania katika tafiti mbalimbali za mafuta na gesi miaka ya 1970.

Kupitia uzoefu wao wa muda mrefu kwenye eneo la nishati, Mhe. Balozi alieleza kuwa yapo mengi ya kujifunza kutoka kwao hususan katika eneo la uzalishaji wa rasilimali watu, tafiti, uzalishaji na usafirishaji wa mafuta, gesi, umeme pamoja na biashara ya nishati.

Katika kutilia mkazo suala la ziama la ushirikiano. Mhe. Balozi alisisitiza kutumia mkataba wa Ushirikiano (MoU) uliopo kati ya TPDC na SONATRACH, TPDC na SONELGAZ uliosainiwa tarehe 01 Agosti 2023 na  kuwa na mpango wa kazi wa utekelezaji wa pamoja na kuwa na ziara kwa pande zote mbili.

Kwa upande wake mkuu wa Msafara na Meneja wa Kanda, Bw. Nteminyanda Kandoro alieleza Dira ya TPDC na mpango wao wa kuongeza uzalishaji wa gesi pamoja na utekelezaji wa sera ya matumizi ya nishati safi nchini. 

Sambamba na hilo, Bw. Nteminyanda aliweka wazi kuwa ziara yao nchini Algeria imelenga zaidi kuimarisha ushirikiano na Algeria na kujifunza  zaidi katika eneo la usimamizi wa rasilimali watu ili kuboresha mazingira ya utendaji na kuongeza ufanisi.

Kwa kumalizia, mkuu wa msafara  aliweka wazi kuwa mbali na kutafuta uzoefu na mafunzo kwenye usimamizi wa rasilimali watu, ziara yao  imelenga kufungua milango  ya ushirikiano kwenye eneo la mafunzo kwa ngazi ya wataalamu.