Tarehe 11 Julai 2025, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai alipokea ujumbe wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ukiongozwa na Mkurugenzi wa Bodi, Balozi Mstaafu Maj. Jen. Jacob Kingu pamoja na wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya REA ambao waliwasili nchini Algeria kwa ajili ya ziara ya kimafunzo.

Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea Taasisi mbalimbali za Shirika la Umma la Umeme na Gesi la Sonelgaz ikiwemo Vituo vya mafunzo, Vituo vya usambazaji umeme na gesi, vituo vya uzalishaji nishati ya umeme na gesi pamoja na kutembelea viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya umeme vinavyomilikiwa na Shirika hilo.

Aidha, kupitia mkutano mkuu kati ya SONELGAZ na REA uliofanyika katika Makao makuu ya Sonelgaz jijini Algiers, Mhe. Balozi alieleza dhamira ya Tanzania kuimarisha ushirikiano wa nishati na Algeria akitilia mkazo utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kwenye sekta ya nishati uliosainiwa kati ya TPDC, TANESCO na SONELGAZ Agosti 2023.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgaz, Mhe. Mourad Adjal alieleza kuhusu utayari wa Algeria kushirikiana na Tanzania katika eneo la nishati ya umeme na gesi ikiwemo kuwajengea uwezo wafanyakazi, kuongeza ufanisi katika uzalishaji, usambazaji pamoja na uendeshaji na utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali ya pamoja.

Aidha, Mhe. Mourad ameahidi kuwa ujumbe wa Sonelgaz utatembelea Tanzania katika kipindi cha karibuni kwa ajili ya kuangalia maeneo zaidi ya ushirikiano kwa lengo la kufanya kazi pamoja katika kutatua changamoto zilizopo kwenye eneo la umeme na gesi.