Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Asha Rose Migiro alifanya ziara ya kikazi nchini Algeria kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 10 Aprili 2026. Ziara hiyo ililenga kumwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya kuanza kwa vuguvugu la uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Saharawi.
Mhe. Katibu Mkuu aliwasili Algiers alasiri ya tarehe 06 Aprili 2026 na kupokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai na wenyeji wake kutoka Chama Kikuu cha Siasa na Kikongwe kabisa nchini Algeria cha Front Liberation National (FLN).
Tarehe 07 Aprili 2026 Mhe. Katibu Mkuu kabla ya kuelekea Tindouf, Algeria alipata nafasi kutembelea Ofisi za Ubalozi zilizopo jijini Algiers na kupokea taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususan masuala ya ushirikiano kutoka kwa Mhe. Balozi.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi alimueleza Mhe. Katibu Mkuu wa CCM uhusiano uliopo kati ya Serikali mbili na fursa ambazo Ubalozi umekuwa mstari wa mbele kuzinadi na kuona kuwa fursa hizo zinainufaisha Tanzania. Miongozi mwa fursa zilizopo ni ushirikiano katika sekta ya nishati (mafuta, gesi, mbolea na mafunzo). Ushirikiano katika Sekta ya uzalishaji wa dawa za binadamu, ushirikiano katika sekta ya elimu, ushirikiano katika sekta ya ulinzi na ushirikiano katika sekta ya biashara ambayo Tanzania inaweza kuuza mazao yake ya kilimo nchini Algeria.
Mhe. Katibu Mkuu alishirikia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Jamhuri ya Kiarabu ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi tarehe 8 na 9 Aprili 2026 yaliyofinyika katika Jimbo la Auserd liliopo Mkoani Tindouf nchini Algeria.
Madhimisho hayo yalizinduliwa rasmi tarehe 8 Aprili 2026 na Mhe. Rais Brahim Ghali na kuhudhuriwa na Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali kutoka nchi mbalimbali duniani kama vile mataifa ya Amerika ya Kusini (Venezuela, Cuba, Mexico, Nicaragua), Nchi za Baltic (Estonia na Lithonia) Mataifa ya Kusini mwa Afrika (Afrika ya Kusini, Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Kenya) pamoja na mataifa ya Ulaya kama vile Slovenia na Switzerland.
Kupitia hadhara hiyo, Mhe. Katibu Mkuu alipata nafasi ya kusoma hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu na kuwasilisha pongezi na mshikamano kwa Serikali na Watu wa Saharawi kwa maadhimisho ya miaka 50 ambayo yanathibisha ushupavu, uimara na uvumilivu wa hali ya juu wa watu wa Sahara Magharibi katika kutetea na kudai haki yao ya kujitwala.
Kupitia hotuba hiyo, Mhe. Rais ameweka wazi msimamo wa Tanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za amani kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa kupitia maazimio ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Sambamba na kwenda na ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2026 "Afrika We Want" na kutoa wito wa kukomesha Ukoloni Barani Afrika na kuendeleza Umoja na Ushirikiano.
Kadhalika, Mhe. Katibu Mkuu alipata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Brahim Ghali na kuwasilisha salamu za Dkt. Samia Suluhu Hassan. Viongozi hao walikubaliana kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Chama cha Mapinduzi na Front Polisario katika nyanja mbalimbali.
Mhe. Katibu Mkuu alihitimisha ziara yake nchini Algeria tarehe 10 Aprili 2026 ambapo alipata nafasi ya kukutana na Katibu Mkuu wa FLN Mhe. Abdelkarim Benmbarek jijini Algiers. Viongozi hao pia walizungumzia umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa kihistoria na kuanzisha ushrikiano wa pamoja katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo vijana, kiuchumi na kisiasa kwa maslahi ya vyama na nchi mbili kwa ujumla.










