Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai ametembelea Chuo Kikuu cha Ouargla na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo Prof, Halilat Med Tahar pamoja na uongozi wa Chuo hicho tarehe 10 Februari 2026.

 

Lengo la ziara hiyo, lilikuwa ni kuangazia zaidi fursa za ushirikiano hususan mafunzo na tafiti katika fani za mafuta na gesi, umeme pamoja na Akili Unde na matumizi yake kwenye fani za uchimbaji wa mafuta na gesi.

 

Chuo Kikuu cha Ouargla ni miongoni mwa Vyuo Vikuu vichache vinavyofanya vizuri kwenye mafunzo hasa kwenye eneo la mafuta na gesi kwa nadharia na vitendo. Chuo hicho, pia, kinanufaika na uwepo wake kijiografia katika mkoa wenye shughuli nyingi za uchimbaji wa mafuta na gesi nchini Algeria.

 

Kupitia mazungumzo hayo, Mhe. Balozi na mwenyeji wake wamekubaliana kuharakisha ukamilishaji wa makubaliano ya ushirikiano pamoja na Vyuo vikuu vya Tanzania hususan Zanzibar State University na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa program za mafunzo, tafiti na ziara za wakufunzi katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele kwa Tanzania.

 

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Balozi alipata nafasi ya kutembelea Kitivo cha Fasihi na lugha za kigeni na kufanya mazungumzo na Mkugenzi Mkuu Prof. Houcine Dahou pamoja na uongozi wa kitivo hicho.

 

Kadhalika, viongozi hao wamekubaliana kusukuma mbele ushirikiano kati ya Kitivo cha Fasihi na lugha za kigeni na upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kwa kukamilisha rasimu za ushirikiano zilizopo ili kusainiwa mapema iwezekanavyo.

 

Mhe. Balozi alihitimisha ziara yake kwa kutembelea madarasa mbalimbli ya wanafunzi wa shahada ya kwanza wa mafunzo ya lugha na Ukalimani.